Mchungaji Lwakatare Aivimbia Serikali.....Apinga Nyumba yake Kubomolewa
Mchungaji
a Kanisa la Assemblies of God,Mikocheni, Dr Getrude Lwakatare
amepinga nyumba yake kubomolewa ikiwa ni siku chache baada ya
wizara ya maliasili na utalii kupitia wakala wa misitu Tanzania
(TFS ), kuweka alama ya X wakidai imo katika hifadhi ya bahari.
Mwishoni
mwa mwaka jana, Serikali ilianza ubomoaji wa nyumba zote zilizojengwa
mabondeni, kama Bonde la Mto Msimbazi, kingo za mito, fukwe za bahari,
pia maeneo ya wazi na hifadhi za barabara, kabla haijasitisha mchakato
huo Desemba 22 na kutoa siku 14 zitakazoisha Januari 5 kwa wamiliki
wenyewe kuzibomoa ili kuokoa mali na baadhi ya vifaa muhimu.
Licha
ya kuwakumba watu wenye vipato vya chini hasa wale waliojenga maeneo
hatarishi, operesheni hiyo imewahusu watu wenye ‘mahekalu’ na majengo ya
biashara kama hoteli na maduka makubwa.
Akizungumza
jana kwa niaba ya mteja wake, wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya
Msemwa & Company Advocates, Jerome Msemwa alizitaka mamlaka
zinazohusika kuheshimu haki za binadamu ambao wanajali sheria za nchi,
kabla ya kutekeleza mambo yao binafsi.
“Jengo
la mteja wangu limewekewa alama X ili libomolewe. Lakini ujenzi wa
nyumba hiyo ulishajadiliwa na kesi yake kuhukumiwa na Mahakama Kuu
kitengo cha Ardhi na akaonekana hakuvunja taratibu zozote za ujenzi.
Hukumu ilitolewa Mei 22 mwaka jana na nakala ipo,” alisema Wakili Msemwa.
“Ubomoaji
huo ni batili na tunaziomba mamlaka zote zinazhohusika kuheshimu hukumu
iliyotolewa, na endapo utekelezaji huo utafanywa itakuwa ni ukiukwaji
mkubwa wa haki.
"Jengo la mteja wangu lina thamani kubwa na hana mahali pa kwenda likivunjwa.”
Nyumba
iliyowekwa alama hiyo imejengwa Mbezi Beach, pembezoni mwa Bahari ya
Hindi, lakini imejengwa kwenye hifadhi ya mikoko hivyo kukiuka matakwa
ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc).
Lakini
Msemwa alisema tayari baraza hilo lilimalizana na mteja wake tena
kisheria katika chombo chenye mamlaka kamili, hivyo kuliibua tena wakati
huu huku maandalizi ya ubomoaji yakiwa yameshakamilika ni kwenda
kinyume na agizo lililotolewa na mhimili huo wa dola.
Wakati
Msemwa akisema kuwa tayari walishamalizana na Nemc, mwanasheria wa
baraza hilo, Manichare Heche alisema kama wana kibali cha kumalizana na
baraza hilo, waonyeshe.