Mbunge wa Kinondoni Mhe. Maulid Mtulya Awasilisha Pingamizi Mahakamani kuhusu Zoezi la Bomoabomoa Katika Jimbo Lake.
Mbunge
wa jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia amewasilisha mahakamani shauri la
kupinga zoezi la ‘bomoabomoa’ linaloendelea jijini Dar es Salaam.
Shauri hilo lenye uwakilishi wa wananchi nane linatarajiwa kusikilizwa katika mahakama Kuu kitengo cha Ardhi, leo (Januari 4).
Kwa
mujibu wa Mtulia, Shauri hilo lilifunguliwa mahakamani hapo Desemba 22
na kupata faili rasmi Desemba 28 mwaka jana. Katika shauri hilo,
walalamikaji wanaiomba mahakama kuamuru usitishwaji wa zoezi la
bomoabomoa ili kuwapa muda zaidi wananchi kujiandaa kupisha maeneo hayo
lakini pia kuwatafutia makazi mbadala.
“Kimsingi
tunachokiomba sisi ni kwamba suala la ubomoaji kwanza lianze na
mazungumzo kwamba kila mtu alipwe haki yake ndipo ubomoaji ufanywe. Na
wananchi wa mabondeni wasitolewe muhanga. Na ninashukuru kwa sababu
serikali imesema inasimamia sheria basi naamini kwa kwenda mahakamani
basi sheria itafuata mkondo wake,” alisema Tulia.
Shauri lililofunguliwa mahakama kuu ni shauri dogo linalofahamika kama ‘Miscellaneous land application’ namba 822 ya mwaka 2015.