MAKOCHA SITA WAJITOKEZA SIMBA


MAKOCHA sita kutoka nchi za Zambia, DR Congo, Uganda, Kenya, Ethiopia na Denmark, wametuma wasifu wao (CV) kwa uongozi wa Simba kuomba kazi ya kuifundisha timu hiyo kurithi mikoba ya Dylan Kerr aliyetimuliwa hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe, alisema jana kuwa hivi karibuni wataanza kuzipitia CV hizo ili kujua kocha gani atakayewafaa.
“Tumeandaa utaratibu maalumu kuwashirikisha wataalamu ili kuweza kupata kocha bora atakayetupa mafanikio na kuturudisha kwenye ushindani wa Ligi Kuu,“ alisema Hans Poppe.
Alisema wanahitaji kocha atakayekuwa na viwango vya kimataifa zaidi, mwenye kulijua vizuri soka la Afrika, pamoja na mazingira wanayoishi wachezaji wake, hivyo anaamini katika CV zilizopo ofisini kwao wanaweza kupata mwenye sifa wanazozihitaji.
Alisema wamechoshwa kuona timu yao ikikosa ubingwa katika misimu mitatu iliyopita na wanachotaka kuanzia msimu huu kuwa na benchi imara la ufundi ambalo litaweza kusimamia vizuri uwajibikaji wa timu na wachezaji ili ufikia malengo wanayoyahitaji.
Alisema wamemchukua Jackson Mayanja, kuwa Kocha Msaidizi kwa kuwa wanajua uwezo wake wa ufundishaji aliokuwa nao na wanachotaka kumletea mtu wa juu yake ambaye watasaidiana kutumia uwezo waliokuwa nao kuifanya Simba kuwa timu inayotisha.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.