MAGUFULI KIBOKO
Siku 70 Ikulu apanda ndege mara moja, Ametoka nje ya Dar mara mbili tu
Desemba 5, 2015, Rais Magufuli hakupanda ndege pia kwenda
Johannesburg, Afrika Kusini kulikokuwa na mkutano wa tano wa wakuu wa
nchi za Afrika na Rais wa China, Xi Jinping, kupitia Jukwaa la Nchi za
Afrika na China (FOCAC). Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwakilishwa
na Makamu wa Rais, Samia Suluhu.
Rais John Magufuli.
Wakati, Rais John Magufuli, akifikisha siku ya 70
ofisini leo tangu kuapishwa kwake Novemba tano mwaka jana, gazeti hili
limebaini kuwa mpaka sasa amepanda ndege mara moja tu na kutoka nje ya
jiji la Dar es Salaam mara mbili tu.
Taarifa hizo ambazo zilithibitishwa na mmoja wa wasaidizi wa Rais
Magufuli, zinaeleza kwamba, jana ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza
kupanda ndege tangu aingie madarakani.
Katika safari yake ya jana, Rais Magufuli alitumia ndege kutoka Dar
es Salaam kwenda Zanzibar kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 52
ya Mapinduzi ya visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa kikokotozi cha mtandaoni (Distance calculator), umbali wa kutoka Dar es Salaam mpaka Zanzibar ni kilomita 73.43.
Muda wa kutoka Dar es Salaam kwa ndege kwenda Zanzibar, kikokotozi
hicho kinaonyesha ni dakika 14 mpaka dakika 20 kutegemea na ukubwa wa
ndege na mwende kasi inayotumia.
Jana Rais Magufuli alikuwa miongoni mwa viongozi wa kitaifa
waliokuwapo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuuungana na Rais Ali
Mohamed Shein katika kusherehekea kilele cha maadhimisho ya sherehe za
Mapinduzi.
Wengine waliokuwapo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa; marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi,
Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid
Amaan Karume.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa, safari iliyomtoa Rais Magufuli
kutoka Magogoni, Ikulu jijini Dar es Salaam hadi Zanzibar ni ya pili
tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015 baada ya kushinda kwa asilimia 58.46
ya kura halali zilizopigwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25,
mwaka jana.
Mbali na safari hiyo, safari nyingine ni ile aliyotumia usafiri wa
barabara kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kufungua Bunge la 11 na
kupendekeza jina la Waziri Mkuu.
Katika safari hiyo ya Dodoma ambako ndipo makao makuu ya nchi na
kuliko na Ikulu ya pili kwa ukubwa ya Chamwino ukitoa ile ya Magogoni,
Rais Magufuli baada ya kuzindua Bunge Novemba 20, 2015 alikaa kwa siku
kadhaa kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kikokotozi cha umbali, kutoka Dar es Salaam mpaka
Dodoma ni kilomita 583.64 ambazo kwa gari linalotembea wastani wa mwendo
kasi wa kilomita 112 kwa saa, litatumia saa tano na dakika 12 kumaliza
safari hiyo.
Wakati leo akifikisha siku ya 70 ofisini, Rais Magufuli hajawahi
kusafiri nje ya nchi na mara kadhaa amekuwa akitimiza ahadi yake ya
kuhakikisha kuwa mabalozi wa Tanzania katika nje ya nchi wanaliwakilisha
taifa kwenye baadhi ya mikutano ili kuondokana na gharama
zinazoepukika.
“Lazima tukubaliane kuwa katika kubana matumizi kuna faida na
hasara zake, ndiyo maana hata kutosafiri kwake kutakuwa na faida nyingi
lakini kunaweza kuwa na hasara kidogo. Ila lazima tu tukubaliane ukitaka
kwenda mbiguni lazima kwanza ufe, vivyo hivyo ukitaka kubana matumizi
kutakuwa na hasara zake,” alisema mmoja wa wasaidizi wa kiongozi huyo.
Wakati akizindua Bunge, Rais Magufuli alisema safari za nje
zimeligharimu taifa Sh. bilioni 356.3, ambazo kati yake Sh. bilioni
183.1 zilikuwa kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh. bilioni 68.6
ziligharamikia mafunzo na Sh. bilioni 104.5 zilikuwa za posho.
Rais Magufuli ambaye amebana safari za nje za watumishi wa umma,
aliliambia Bunge kwamba, fedha hizo zingeweza kujenga kilometa 400 za
barabara ya lami.
Licha ya safari hizo za kikazi, Rais Magufuli pia alisafiri kutoka
Dar es Salaam hadi Msoga, mkoani Pwani kwenye msiba wa dada wa Rais
Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Mpaka sasa, licha ya watumishi wengi wa serikali kuomba kusafiri
nje ya nchi na kunyimwa kibali, serikali imewasimamisha kazi watumishi
wanne wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kwa kwenda
nje ya nchi bila kibali maalumu cha Ikulu.
Itakumbukwa pia kuwa, mpango wa Rais Magufuli wa kubana matumizi,
ulifanya utaratibu wa kusherehe siku ya Uhuru ibadilishwe na watu
kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi badala ya kwenda uwanja wa taifa
kuangalia gwaride na halaiki ambayo huwa inagharimu mabilioni.
Kutokana na kuahirishwa kwa shamrashamra hizo, Sh. bilioni nne
zilizookolewa na kuelekezwa kwenye utanuzi wa barabara ya Bagamoyo eneo
la Mwenge mpaka Morocco ambako kazi hiyo inaendelea kwa sasa.
Mpango huo wa kubana matumizi ya serikali, pia ulifanya sherehe ya
kufungua Bunge ifutwe na fedha zake kuelekezwa kununua vitanda vya
wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Hatua ya Rais Magufuli kutosafiri mara kwa mara huku pia serikali
yake ikidhibiti safari za nje kwa viongozi na watumishi wote wa serikali
imekuwa ikiwavutia watu wengi nchini na kwingineko nje ya Tanzania,
akiwamo mgombea urais wa upinzani nchini Uganda, Dk. Kizza Besigye.
Katika moja ya mikutano yake ya kampeni akiwa kwenye wilaya ya
Agago, nchini humo, Besigye alisema akiingia Ikulu atafuata nyayo za
Rais Magufuli kwa kupiga marufuku safari holela za nje ya nchi na
kuongeza kuwa ataiuza ndege anayoitumia mpinzani wake, Rais Yoweri
Museveni, aina ya Gulfstream V Jet.
Licha ya rekodi ya Rais Magufuli ya kutosafiri kwenda Ulaya na nchi
nyingine za nje ya Tanzania hata mara moja tangu aingie madarakani
kuwavutia wengi, baadhi ya watu waliozungumza na Nipashe wamedai kuwa
hali hiyo ni balaa kubwa la kiuchumi kwa wasaidizi wa Rais ambao wengi
wangetamani asafiri zaidi kama ilivyo kwa wakuu wengine wengi wa nchi za
Kiafrika waingiapo madarakani.
Kutokana na rekodi ya safari za Magufuli, ni wazi kuwa hadi sasa,
wasaidizi wa Rais huyo wa awamu ya tano watakuwa wamehusika katika
safari za kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea kwenye Ikulu ndogo ya
Chamwino, Dodoma na Unguja visiwani Zanzibar alikokuwa jana.
“Rais yeyote anaposafiri ni lazima aambatane na timu ya watu kadhaa
wa karibu yake. Kama Rais anasafiri mara kwa mara, ni wazi kwamba hawa
pia hunufaika kwa safari hizi ambazo huambatana na posho nzuri za
safari. Hata hivyo, kwa hawa (wasaidizi) wa Rais Magufuli hali iko
tofauti… Rais amesafiri mara chache na hivyo wao pia watakuwa wameguswa
na ratiba hiyo kwa kusafiri mara chache,” chanzo kimoja kiliiambia
Nipashe jana kuhusiana na safari za Rais.
SAFARI ALIZOJIKOSESHA MAGUFULI
Pengine katika kutekeleza agizo alilolitoa la kudhibiti safari za
nje, Rais Magufuli hakusafiri kwenda kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa
Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika visiwa vya Malta Novemba 27,
mwaka jana.
Badala yake, Rais Magufuli alimtuma Balozi wa Tanzania nchini
Uingereza kwenda kumwakilisha katika mkutano huo, akiwa pamoja na
maofisa wengine watatu na hivyo jumla yao kuwa watu wanne. Inaelezwa
kuwa wakati wa utawala wa awamu ya nne, msafara kwenye mkutano kama huo
uliofanyika Malta ulikuwa ukimhusisha Rais, baadhi ya mawaziri na
maafisa wengine wa juu serikalini ambao kwa ujumla walikuwa takribani
50.
Novemba 29, mwaka jana, Rais Magufuli alitakiwa kuwapo jijini
Paris, Ufaransa katika mkutano wa kimataifa wa 21 kujadili mabadiliko ya
tabianchi duniani (COP21) ambapo wakuu wa nchi takriban 150 kutoka
katika nchi 195 walishiriki, wakiwamo marais Barack Obama wa Marekani na
Xi Jinping wa China. Hata hivyo, hakukwea ndege kwenda kuhudhuria
mkutano huo na badala yake akabaki nyumbani akiendelea kushughulikia
‘upasuaji majipu’, hasa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Bandari
(TRA).
CHANZO:
NIPASHE