Maalim Seif Kupasua Jipu Leo

Hii ni habari inayopewa nafasi ya kwanza na mtandao wa Jamjicho Blog.Maalim Seif ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Katika sintofahamu iliyopo sasa kwa muda mrefu hajanukuliwa akitoa kauli. Tayari msimamo wa CCM Zanzibar umefahamika, kuwa wako tayari uchaguzi urejewe. CUF wao wanasikika wakiweka msimamo kuwa wao ndio washindi, watangazwe tu.
Katika hili wa kutangaza hilo ni Tume, na ni Tume hiyo hiyo iliyoyafuta matokeo na maamuzi kuchapwa kwenye gazeti la Serikali. Hilo likitoa tafsiri kuwa Tume haiwezi katika mazingira ya sasa kuyapitia upya maamuzi ambayo inadai yamefanyika kisheria.
Maalim Seif kwa kuongea na Wahariri leo anamtangulia njiani Dr Shein kwa hotuba yake ya kesho kwa Wazanzibar kupitia maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi. Kauli ya Maalim Seif leo itatoa mwanga wa Wazanzibar wanakokwenda.
Tumepata kulitolea maoni hili, kuwa, katika mazingira ya sasa, hekima na busara ikitangulizwa, hakuna namna yeyote ile nyingine kwa Wazaznibar kusonga mbele bila kukubaliana kwa pamoja, kuwa wanarejea uchaguzi chini ya taratibu na uangalizi usio tia mashaka ya pande mbili kuchezeana rafu mbaya. Matokeo ya uchaguzi kwenye uchaguzi huo lazima yaheshimiwe na pande zote mbili na yatapelekea kuunda Serikali nyingine ya Umoja wa Kitaifa, maana, kwa Zanzibar ilivyo sasa, na kwa Katiba yao mpya inavyoruhusu, muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa- GNP ni tiba mujarab kwenye yenye kuwasibu Wazanzibar.


Theme images by hanoded. Powered by Blogger.