LOWASSA AIPA JEURI UKAWA,MENGI YAFICHUKA


Wakati katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akitangaza kujiondoa chama hicho, aliacha maswali ya kutathmini ujio wa Edward Lowassa kama utakuwa mzigo au mali kwa vyama vya upinzani, na sasa wilaya za Ilala na Kinondoni zimekamilisha majibu.


Ushindi wa kwanza wa vyama vya upinzani katika nafasi ya umeya za manispaa hizo mbili umeonyesha nguvu ya waziri huyo mkuu wa zamani aliyotoka nayo chama tawala.
Ushindi huo ambao unavifanya vyama vya Chadema na CUF kuelekea kutwaa umeya wa Jiji la Dar es Salaam, pamoja na mwingine kwenye majiji ya Mbeya na Arusha umedhihirisha nguvu ya Lowassa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine vitatu, CUF, NLD na NCCR Mageuzi vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Lowassa ameiteka Dar,” alisema Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kwenye mahojiano na gazeti la Mwananchi kabla ya madiwani wa CUF na Chadema kushinda viti vya umeya wa Ilala na Kinondoni mwishoni mwa wiki.
“Tangu upinzani uingie nchini haujawahi kuishika Dar.”
Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki, alisema Lowassa ameweza kuvipa vyama hivyo nafasi ya kuongoza halmashauri jambo ambalo linathibitisha kuwa alikuwa ni mali na si mzigo kwao.
Katika uchaguzi wa meya wa Manispaa ya Kinondoni, diwani wa Ubungo, Boniface Jackob alishinda kwa kupata kura 38, huku Jumanne Mbulu wa CUF akitwaa unaibu meya. Kwenye Manispaa ya Ilala, Charles Kayeko (Chadema) alishinda umeya na Omari Kumbilamoto wa CUF alitwaa unaibu.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa vyama vya upinzani jijini Dar es Salaam tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.
Mbali na ushindi huo, Ukawa imefanikiwa kutwaa viti kadhaa kwenye halmashauri ambazo zilikuwa mikononi mwa CCM hivyo kuongeza wigo wao kwenye uongozi.
Mkoani Kilimanjaro, Chadema imeshika halmashauri sita kati ya saba ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Rombo, Moshi Vijijini na Siha wakati mkoani Mbeya, Chadema imechukua halmashauri ya jiji hilo, pamoja na ile ya mji wa Tunduma.
Mkoani Arusha na Manyara, Chadema na Ukawa zimechukua Halmashauri ya Jiji la Arusha, Monduli, Karatu, Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi na Babati Mjini, wakati mkoani Kagera Ukawa imechukua Manispaa ya Bukoba na mji mdogo wa Kayanga.
Mkoani Mtwara, CUF na Ukawa zimechukua halmashauri ya Tandahimba, Mtwara Mjini na Newala Mjini huku mkoani Lindi ikichukua Kilwa.
Mkoani Mara, Chadema kupitia Ukawa inaongoza halmashauri ya Serengeti, Tarime Vijijini na Tarime Mjini.
Mkoani Morogoro, Ukawa imechukua halmashauri ya Kilombero na Ifakara huku mkoani Iringa ikichukua ile ya Iringa Mjini.
Kwa mujibu wa Lissu ongezeko la halmashauri kuwa chini ya wapinzani limechangiwa na waziri huyo mkuu wa zamani aliyejiuzulu mwaka 2008.
Alipoulizwa kuhusu nguvu hiyo ya Lowassa, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli ameleta chachu ya kupata madiwani na wabunge wengi ingawa muungano wa Ukawa nao umesaidia.
“Ukawa ndiyo kiini cha mafanikio, lakini chachu kubwa ni Lowassa kujiunga na Chadema kwa kuwa alikuwa na wafuasi wengi,” alisema Profesa Mpangala.
Alisema hata kusingekuwa na Ukawa wala Lowassa kujiunga na Chadema, Chadema imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka kwa kuongeza idadi ya wawakilishi katika uchaguzi.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.