Kuna Watu Bado Wanaamini Kuna Mabadiliko Chini ya CCM? Basi Soma Hii
Nimetazama sana hizi siku 60 na ushee za mh. Rais Magufuli nimejikuta naanza kuendelea kuamini hakuna mabadiliko ya dhati yanayoweza kuletwa chini ya uongozi wa CCM.
Ndani ya siku 60 tu tumeshuhudia akifanya makosa ambayo ni "grave mistakes". Hebu tuyatazame kwa uchache.
1. CCM imeingia ktk uchaguzi mkuu ikiwa na harufu mbaya ya ESCROW, bunge likapitisha maazimio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha watendaji na viongozi waandamizi waliohusika ambao wameteuliwa na rais, hapo ndipo prof. Mwijarubi Muhongo na bwana Eliakimu Maswi walitakiwa wawekwe kando.
Cha ajabu teuzi za mh. Magufuli amewarudisha hawa waliobariki wizi ule, hii inanipa dhana tatu.
(a)Huenda madai ya wapinzani wakati wa kampeni kuwa pesa ya Escrow zimekwenda kugharamia kampeni za CCM?
(b)Bunge kama muhimili wa dola umepoteza sifa na heshima yake, kwani hiyo ni dharau dhidi ya taasisi ya bunge.
(c)Hakuna wizi ambao unatendeka pasi na CCM kufahamu hivyo wapinzani tu ndio wenye viherehere vya kukata mrija wa pesa kwa "miungu watu".
2. Bomoa bomoa inayoendelea sasa jijini Dar es Salaam huku kukiwa na malalamiko lukuki lakini taasisi kubwa kama ikulu imekaa kimya.
Mengi yatajadiliwa lakini serikali ni kama baba wa wananchi. Ilipaswa kuwahamisha kiustaarabu na kuwaonesha mahala pa kujihifadhi lakini pia kwa kutumia njia ya majadiliano na ikibidi kuwalipa fidia wananchi.
Mwananchi kajenga nyumba yake kwa miaka 5, serikali inakuja inatoa notice ya miezi mitatu au isitoe kabisa, je serikali ilikuwa usingizini wakati wote huo?
3. Kudhalilisha na kuwatisha watumishi wa umma. Tumeshuhudia ndani ya siku 60 watumishi wa umma wakinyimwa likizo, wakikataliwa kusafiri, wakisimamishwa kazi pasi na kufuata taratibu za kiutumishi wengine wakidhalilishwa mahakamani kwa kesi ambazo kwa nje kuna baadhi unajua serikali itashindwa.
Nieleweke wazi hapa, kwa mwananchi wa kawaida tunaona kama faraja kwetu watumishi wa umma wanavyodhalilishwa kwani tunaamini maisha yetu magumu yameletwa na uzembe wao.
Lakini ukifikiri kwa mapana utagundua kuna haja ya kuchunguza badala ya kudhalilisha watumishi kwenye media ili kujiongezea umaarufu wa kisiasa.
4. Siku ya usafi yaani 9 desemba. Kwa kufuata agizo lake nchi nzima ikajikuta ikiingia ktk zoezi hili kwa kulazimishwa, kweli watu walishika fagio wakaingia kufagia barabarani(na sio maeneo ya makazi) na matokeo yake pia taka zote zikatolewa kwenye mitaro na kuwekwa barabarani pasi na kuzolewa.
Haya ni matokeo ya kutoa maagizo ya kibabe, wananchi walitenda usafi kwa "agizo" na sio kwa kupewa elimu ya usafi na wakafanya huku wakijua faida za usafi.
5. Kubebana kwa wateule, hivi kuna mtu alitarajia January Makamba, William Lukuvi, na msururu wa makatibu wakuu kama wanaweza wakarudi tena ktk utawala?
Sawa, ni "maamuzi ya rais" na hakuna anayeweza kuyazuia.
Kwa mawazo yangu huru, kwa siku 60 sijajutia kumpa kura yangu Edward Lowassa, labda huko mbele. Tungoje.
Shukrani A. Ngonyani,
januari 5, 2016.
Tanga,
00255784379799,
sirngonyani@gmail.com