KESI YA KUBENEA IMEFIKIA HAPA


Mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea.
 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imesema itaanza kusikiliza ushahidi wa Jamhuri dhidi ya Mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea, Februari 8 na 9, mwaka huu.
 
Hatua hiyo ilifikiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa jana lakini shahidi hakufika mahakamani hapo.
 
Wakili wa Serikali Mwandamizi Credo Lugaju alidai kuwa kesi ilipangwa kusikilizwa Januari 20 na 21, mwaka huu, ushahidi wa Jamhuri lakini upande wa Jamhuri haukuwa na shahidi na uliomba tarehe nyingine ya kusikiliza.
 
Hata hivyo, wakili wa utetezi Peter Kibatala alidai kuwa mshtakiwa anatakiwa kuhudhuria vikao vya kamati za bunge mjini Dodoma, aliomba kesi hiyo ipangwe mwezi Februari.
 
Hakimu Simba alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa Februari 8 na 9, mwaka huu na dhamana ya mshtakiwa inaendelea.
 
Katika kesi ya msingi, Kubenea anadaiwa kuwa Desemba 14, 2015, katika Kiwanda cha nguo cha TOOKU kilichoko Mabibo External, Dar ves Salaam, Kubenea alitumia lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, hali ambayo ingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
 
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Kubenea alimwambia Makonda; “wewe kibaka, mpumbavu, mjinga na cheo chenyewe cha kupewa tu,” ulinukuu upande wa Jamhuri.
 
CHANZO: NIPASHE
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.