Halmashauri yasalimu Amri kwa Madiwani wa Ukawa

Halmashauri ya Jiji la Tanga imesalimu amri kwa madiwani wa Ukawa waliokuwa wakipinga uundwaji wa kamati za baraza hilo kwamba zimeundwa kinyemela ambapo Kaimu Mkurugenzi amekubali kusitisha chaguzi za wenyeviti wa kamati hadi hapo taratibu zitakapo kamilika.


Halmashauri hiyo iliunda kamati za baraza hilo ambazo madiwani wa Ukawa walizikataa wakidai zimeundwa kinyume na sheria ya TAMISEMI na kulazimika kuunda tume ya kutaka ufafanuzi kwa Mkurugenzi huyo kwa kuwa hana mamlaka ya kufanya hivyo.


Uchunguzi uliyofanywa na Nipashe ulibaini kuwa siku moja baada ya kaimu mkurugenzi huyo, Dk Wedson Sichalwe kukutana na tume hiyo na kufanya mazungumzo nayo aliandika barua kwa wajumbe kusitisha zoezi la
uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo.


Hali hiyo ilielezwa kama ni ushindi wa tume hiyo ambayo licha ya kupinga kamati hizo lakini pia ilimtaka asimamishe zoezi la chaguzi za wenyeviti wake na kuitisha kikao halali chenye mamlaka kisheria ya kuunda kamati hizo.
Hata hivyo Dk Sichalwe alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na sakata na mkanganyiko wa uundwaji wa kamati hizo, aling’aka na kudai kuwa licha ya kuwa Kaimu Mkurugenzi lakini hana mamlaka ya kuelezea kilichojiri ndani ya kamati hizo kwa kuwa hairuhusiwi kisheria.


“Unajua hata huyo aliyekueleza amekiuka kanuni na anastahili kuchukuliwa hatua, vikao vya kamati hizi ni vikao vya ndani na ni mwiko kwa mtu yeyote kuyatoa nje ya kikao mambo yaliyozungumzwa humo kwa sababu hiyo mimi sina mamlaka kufanya hivyo na mimi nitakuwa nimekiuka” alisema Dk Sichalwe.


Aidha alibainisha kuwa kilichozungumzwa ndani ya kikao hicho kinamanufaa kwa halmashauri,jamii na taifa kwa ujumla na kutoa wito kwa wapenda maendeleo wa Tanga kuvuta subra ili taratibu zinazofanywa ziweze kuleta matunda.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.