CUF Yanyooshewa Vidole Zanzibar
VYAMA vya siasa visiwani Zanzibar vimeshutumu uamuzi wa Chama cha Wananchi (CUF) kususa sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema kimedhihirisha kilivyo na kigugumizi kutambua mapinduzi ya mwaka 1964.
Viongozi wa vyama vya Tadea, AFP na Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliozungumza kwa nyakati tofauti, baadhi wameeleza kushangazwa na sherehe hizo za kitaifa kuhusishwa na itikadi ya vyama vya siasa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kwa muda mrefu CUF na viongozi wake walisusia sherehe za Mapinduzi kabla ya kuja kwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Alisema kwa muda mrefu viongozi wa chama hicho walikuwa wakipinga na kutaka neno SMZ likimaanisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lisitumike kwa sababu ya kuchukizwa na Mapinduzi.
“Mimi chama cha CUF kususia sherehe za miaka 52 ya mapinduzi ya Zanzibar si kitu kigeni hata kidogo kwa sababu viongozi wa chama hicho kwa muda mrefu walikuwa wakipata kigugumizi kuyatambua Mapinduzi hayo ambayo baadhi yao walidiriki kusema kwamba ni umwagaji wa damu,” alisema Vuai.
Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha AFP, katika uchaguzi uliofutwa, Said Soud alisisitiza kuwa sherehe za Mapinduzi kwa sasa ni za kitaifa na hazipaswi kuhusishwa na itikadi ya vyama vya siasa.
Soud alisema sherehe hizo ni utambulisho wa wananchi wa Zanzibar walivyojikomboa na utawala wa Kisultani . Alisema zinatakiwa kuenziwa na kutunzwa na si kubezwa kama walivyofanya viongozi wa CUF.
“Hawa viongozi wa CUF wanatakiwa kurudi darasani kupewa elimu ya uraia ile iliyokuwa ikitolewa na Redet kuhusu kujua wajibu wa mwananchi na taifa lake na sio kubeza mafanikio ya uhuru,” alisema.
Wakati huo huo Tadea kupitia kwa Juma Khatib aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar uliofutwa, alisema kitendo kilichofanywa na CUF kususia sherehe za Mapinduzi kimeleta picha mbaya na kujaribu kupandikiza mbegu ya chuki kwa kizazi kijacho.