BREAKING NEWZZ: VIGOGO WENGINE WA SERIKALI WASIMAMISHWA KAZI, MAJINA YAO HAYA HAPA.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa George B.
Simbachawene (Mb) amewasimamisha kazi Wakurugenzi Watendaji wa Manispaa
za Kigoma, Mkoa wa Kigoma na Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi kwa
tuhuma za kuridhia na kutekeleza maamuzi ambayo yamesababishia Serikali
hasara na upotevu wa fedha.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Wizara hiyo iliyotolewa leo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Mhandisi
Boniface Nyambele anakabiliwa na tuhuma ya uuzaji wa nyumba za
Halmashauri bila kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo na bila kibali cha Waziri Mwenye Dhamana kama Sheria inavyo elekeza.
Taarifa imesema kuwa
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Ndugu Suleiman Lukanga ana kabiliwa na
tuhuma za Ununuzi hewa wa gari la kusomba taka kwa kiasi cha shilingi
milioni tisini na mbili na laki saba na elfu hamsini (92,750,000/=) na
ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Kakese kiasi
cha shilingi milioni mia mbili, tisini na nne (294,000,000/=).
Aidha, taarifa inasema
Mheshimiwa Waziri wa Nchi ameagiza nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya
Kigoma ikaimiwe na Mhandisi Sultan Imari Ndilowa ambaye ni Mkuu wa Idara
ya Maji, Manispaa ya Kigoma, nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda
ikaimiwe na Ndugu Lauteri John Kanoni ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Waziri wa Nchi,
amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote
Nchini kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao wafuate Sheria,
Kanuni na Taratibu zilizopo. Serikali haitasita kuchukua hatua za
kinidhamu kwa watumishi wote ambao watakiuka matakwa ya Sheria, Kanuni
na Taratibu na kutoweka mbele maslahi ya Umma.
