BREAKING NEWS: WATUMISHI SABA WASIMISHWA KAZI
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera wamewasimamisha watumishi saba wa idara mbalimbali katika halmashauri hiyo ili wapishe uchunguzi zaidi juu ya tuhuma zinazowakabili za kuhusika na ubadhilifu wa fedha za umma.
Mwenyekiti iliyobaini ubadhilifu wa fedha Halmashauri ya Bukoba Wambura Sabora
Watumishi waliosimamishwa ni pamoja na Mtunza hazina , Jonathan Katunzi , Selialis Mutalemwa, Mhasibu, Mhandisi wa idara ya Ujenzi Robert Massoro na Deus Buzibu, afisa elimu wa sekondari Lucas Mzungu, mkuu wa idara ya mifugo Dkt. Kisanga Makinga na Mustapha Sabuni ambaye ni mkuu wa idara ya mipango.
Madiwani hao wamefikia uamuzi wa kuwasimamisha watumishi hao baada ya kupokea na kujadili taarifa ya kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa Kagera John Mongela iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Wambura Sabora iliyobaini ubadhilifu wa fedha za mfuko wa jimbo, fedha za afya, fedha za ujenzi wa barabara na fedha za kiinua mgongo kwa madiwani waliomaliza muda wao na posho zao.
Kufuatia uamuzi wa madiwani hao mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongela ameviagiza vyombo vya dola mbavyo ni pamoja na idara ya usalama, jeshi la polisi na taasisi ya kuzua na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kufutilia undani wa tuhuma zinazowakabili watumishi hao, pia ameagiza ufanyike ukaguzi maalumu utakaosimamiwa na ofisi na mkaguzi na mdhitibi wa hesabu za serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Murshid Ngeze akizungumza baada ya madiwani kufikia uamuzi wa kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi hao ameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na mkuu wa mkoa wa Kagera , John Mongela za kuwashughulikia wanajihusisha na vitendo vya ubadhilifu wa fedha za umma mkoani humo.