BREAKING NEWS : WALIOKAIDI AMRI YA RAIS MAGUFULI BADO WANAISOMA NAMBA,HAKIJAELEWEKA SIRI NZITO YATANDA
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), imesema mchakato wa kinidhamu unaendelea dhidi ya watumishi wake ambao walisimamishwa kazi kwa kukaidi agizo la Rais John Magufuli la kutosafiri nje ya nchi.Jana Nipashe ilifanya mahojiano kwa njia ya simu na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, kuhusiana na hatma ya wafanyakazi hao, ambapo alieleza bado wamesimamishwa kazi na mchakato wa kinidhamu unaendelea.
Alisema tayari watumishi hao walishapewa barua za kujieleza kuhusiana na suala hilo na baada ya kujibu, kamati ya maadili ya Takukuru itakaa na kuona hatua stahiki za kuchukua dhidi yao.
Mlowola alisema bado hawajajua suala hilo litafikia ukomo lini na kwamba watakapokamilisha watatoa taarifa ya kwa vyombo vya habari.
Watumishi ambao walisimamishwa kazi Novemba mwaka jana ni Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha ambao walisafiri nje ya nchi si tu bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, bali pia licha ya kunyimwa ruhusa hiyo.
Muda mfupi tangu kuapishwa, Rais wa Tano, John Magufuli alifuta safari za nje kwa watumishi wa umma zisizo na tija.
Aidha, Katibu Mkuu kiongozi alitoa mwongozo unaoweka masharti ambayo watumishi wa umma wanaotaka kusafiri nje ya nchi watatakiwa kutimiza ili wapewe kibali cha kusafiri.
Sharti la kwanza ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na maombi yawasilishwe kwa Msajili wa Hazina kabla ya kwenda kwa Sefue ili aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu wa safari hiyo na tija itakayopatikana kutokana na safari hiyo.
Sharti lingine linamtaka Mtendaji Mkuu wa Shirika ama taasisi apime kuona kama safari hiyo ni muhimu kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kabla ya kuwasilishwa Hazina na aeleze manufaa ambayo nchi itapata kutokana na safari hiyo.
Pia sharti lingine linataka mhusika aeleze umuhimu wa safari hiyo na isipofanyika itaathiri vipi nchi.
Ofisi za Umma zilipokea barua kutoka kwa Msajili wa Hazina Novemba 12 ikieleza kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla kwa safari za nje ya nchi katika utumishi wote wa umma na mihimili yake. Barua hiyo ya Hazina ilisema zuio hilo litadumu hadi pale itakavyoelekezwa vinginevyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI