BORA YA LOWASSA:MABADILIKO YA RAIS MAGUFULI YAANZA KULETA VILIO KUTOKA KWA WAFANYABIASHARA SOMA HAPA KILIO CHAO LIVE!!
Hatua
ya serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi kwa kuzuia wizara,
taasisi na mashirika ya umma kukutana katika hoteli kwa shughuli
mbalimbali za kikazi, imeanza kuleta athari chungu huku baadhi ya
wamilikiwa hoteli wakisema wameathirika kimapato na sasa wako mbioni
kupunguza wafanyakazi.
Kadhalika,
baadhi ya wasomi wamesema licha ya dhamira nzuri ya serikali katika
kuhakikisha inabana matumizi ili fedha zitakazopatikana zielekezwe
katika miradi ya maendeleo, bado kuna haja ya kuangalia kwa umakini
athari zake. Pia wameonya kuwa sekta ya hoteli ikiyumba itaathiri
wajasiriamali wengi na sekta binafsi kwa ujumla.
Baada
ya kuapishwa na kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, Rais Dk.
John Magufuli ilitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi yasiyo ya
lazima ili kuipa nguvu ya kuwatumikia wananchi.
Miongoni
mwa hatua zilizochukuliwa ni ni kupiga marufuku vikao vya kazi vya
taasisi na mashirika ya umma kufanyika hotelini, kufanyika kwa hafla za
kupongezana, kuadhimisha wiki mbalimbali zikiwamo za maji na Siku ya
Ukimwi, warsha, semina, makongamano, mikutano na mafunzo.
Zingine
ambazo sasa zinaelezwa kuathiri baadhi ya wajasiriamali na sekta
binafsi ni pamoja na kufutwa kwa sherehe mbalimbali ikiwamo ya Uhuru,
maadhimisho ya kitaifa na kimataifa yaliyokuwa yakiwalazimu wageni
mblimbali kutoka nje ya nchi kutua Tanzania au kusafiri kutoka mkoa
mmoja kwenda mwingine.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa tangu kutolewa kwa agizo la
serikali kuzuia hafla, vikao na shughuli za serikali kwenye kumbi za
hoteli, karibu hoteli zote hazijapata mikutano wala shughuli yoyote
kutoka kweye taasisi za umma, mashirika wala wizara.
CHAMA CHA WENYE HOTELI
Mkurugenzi
Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Latifa Sykes,
alisema sekta ya hoteli ni moja ya maeneo yanayoajiri watu wengi kwa
sababu ya kuangalia wageni na kushughulikia matukio mbalimbali, ikiwamo
mikutano.
“Kitu
kitakachotokea na ambacho kwa sasa kinatokea ni kwamba hoteli za mjini
ambazo zilikuwa zikipokea mikutano mingi, sasa zitapunguza wafanyakazi,”
alisema.
Alisema
mbali na kupunguzwa kwa watu na pato la hoteli hizo kupungua,
kutaathiri pia serikali kwa sababu ilikuwa ikipata kodi mbalimbali ikiwa
ni pamoja na ile ya ongezeko la thamani (VAT).
“Lazima
tuwe makini na tujue kila hatua ina matokeo yake. Kwenye hii ya
kupunguza mikutano, matokeo yake ni kupungua kwa mapato yaliyokuwa
yalipwe serikalini na hakuna tena sababu ya kuwa na wafanyakazi wengi.
“Tunamuunga
mkono Rais kwenye kubana matumizi mabaya ya serikali lakini ni vyema
akaangalia hatua za utekelezaji zisiathiri uchumi na biashara
zinazosaidia ukusanyaji wa kodi,” alisema.
HALI HALISI
Ofisa
Mauzo wa hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro Kempinsk), Godlove
Mlaki, aliiambia Nipashe kuwa agizo la Rais Magufuli halijawaathiri
sana kwa sababu hawategemei mikutano pekee ya serikali na taasisi zake
kwa kuwa hoteli yao ni ya hadhi ya kimataifa.
Alisema
athari ya moja kwa moja waliyopata kutokana na uamuzi wa serikali ni
kukosa wateja ambao kwa kawaida huwapata wakati wa maadhimisho ya siku
ya Uhuru, Desemba 9 ya kila mwaka.
Wakati
wa sherehe za kitaifa, ikiwamo Uhuru, wageni mbalimbali ambao hualikwa
kutoka nje ya nchi wakiwamo na marais na wafanyabishara, hufika kwa
wingi nchini na kusaidia kuingiza fedha za kigeni kutokana na kulala
kwenye hoteli na huduma zingine wanazohitaji katika siku zote
wanazokuwapo nchini.
Mlaki
alisema kutofanyika kwa sherehe za Uhuru kuliwakosesha fedha nyingi kwa
sababu awali hoteli yao ilikuwa ikipokea wageni kutoka nje waliokuwa
wakialikwa kuhudhuria sherehe hizo.
Alisema
hoteli hiyo yenye kumbi 10 za mikutano, wateja wake wakubwa walikuwa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na wastani wa
mikutano waliyokuwa wakifanya kwa mwezi ilikuwa ikifikia 19.
Alisema kuna wakati walikuwa wakipata mikutano ya siku mbili hadi sita mfululizo kutoka serikalini.
“Toka mwaka jana Desemba hadi Januari hatujapata (kuandaa) mikutano yoyote kutoka serikalini,” alisema Mlaki.
Mmoja
wa wafanyakazi wa hoteli hiyo, alisema mbali na wateja wananaotaka
kumbi za mikutano, hata baadhi ya maaofisa wa serikali waliokuwa
wakifika hapo ili kupata kifungua kinywa na chakula cha mchana, siku
hizi hawapo tena.
Akifafanua
juu ya ugeni wa marais waliokuwa wakifika kuhudhuria shehere za
kitaifa, alisema: “Wakija marais wawili tu kwa mfano, ukiweka na walinzi
wao, utakuta umeshafanya biashara ya zaidi ya vyumba 30, hapo hujaweka
chakula na vinywaji. Kwa hiyo ile ni biashara kubwa sana kwetu,”
alisema.
Katika
hoteli ya Bahari Beach, Meneja anayehusika na kukodisha kumbi, Robert
Vitus, alisema wameathirika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa tangu kutolewa
agizo la kuzuiwa kwa vikao na mikutano hotelini, hawajawahi kupata
wateja kutoka serikalini.
Alisema hivi sasa wateja wanaowapata zaidi ni wale wanaotoka katika taasisi na kampuni binafsi pekee.
"Kwa
ujumla, siku zote wateja wetu wakuu ni wale wanaotoka katika taasisi
binafsi na wengine kutoka nje ya nchi. Watu wa serikalini kwa kiasi
fulani walikuwa wateja wetu, japo si kama ilivyo kwa hawa wengine. Hivi
sasa, hata hao asilimia ndogo ya wateja kutoka serikalini hatuwapati
tena," aliongeza.
Meneja
Masoko wa Hoteli ya Blue Pearl iliyoko Ubungo, Abdul Sheikh, alisema
kutokana na serikali kuacha kufanya mikutano kwenye hoteli yao, baadhi
ya wafanyakazi wamekosa kazi za kufanya.
“Yaani
hakuna kabisa biashara siku hizi kulinganisha na ilivyokuwa awali
ambapo kumbi zote zilikuwa zinajaa. Sasa hivi ni kama ulivyotukuta,
hakuna kazi, kuanzia asubuhi hadi jioni, ni hivi hivi tu tunakaa”
alisema Sheikh.
WASOMI WANENA
Mtafiti
wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji
Semboja, alisema ingawa hoteli kadhaa zitakuwa zimeingia katika
msukosuko wa kiuchumi, bado kuna haja kwa serikali kuangalia ushirikiano
mkubwa wa maendeleo baina ya sekta binafsi na ya umma katika kukuza
pato la nchi.
Alisema
kadri anavyoona, agizo la Rais Magufuli, moja kwa moja halikulenga
kusitisha mikutano mikubwa yenye idadi ya watu zaidi ya 200 hadi 500,
bali ile midogo ambayo haikuwa na ulazima wa kufanyika katika kumbi za
hoteli kwa lengo la kuokoa rasilimali fedha ambayo inaweza kufanya jambo
mbadala.
“Kuyumba
kiuchumi kwa hoteli hizo huenda kumechangiwa na uelewa mdogo wa tabia
za Waswahili, ambao wanajumuisha kila kitu na kusababisha hofu
iliyochangia kuyumba kiuchumi kwa sekta binafsi ambayo ni miongoni mwa
mihimili muhimu ya serikali hasa katika uchangiaji wa uchumi wa ndani,”
alisema.
Mkurugenzi
wa Sera wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Kamote,
alisema katika nchi yoyote serikali ni muhimili wa kwanza wa ununuzi wa
bidhaa na huduma, hivyo inavyobana sana matumizi yake itasababisha
kuathirika kwa sekta mbalimbali na kusababisha uchumi mkuu kushindwa
kukua.
“Kubana
bajeti ni jambo la kawaida, ila ibane na kuachia ili kutoa ushirikiano
mzuri kwa sababu inaweza kusababisha madhara kwa sekta iliyodhamiria
kuibana. Tunajua inaweza kubana na fedha zile zikatumika katika sekta
nyingine kama elimu au afya,” alisema Kamote.
Alisema
ni vigumu hoteli nyingi kumudu kujiendesha bila kupata mteja muhimu
ambaye ni serikali, hasa kwa sababu serikali imeanza kwenye eneo
linalogusa sekta ya utalii ambayo ni kitovu kikubwa cha uchumi.
Alisema
huenda ajira nyingi kwa wafanyakazi wa hoteli zikapungua huku wengi
wasijue la kufanya na kujikuta wakiangukia katika kundi la wazururaji au
shughuli haramu kama za utapeli.
IKULU YAFUNGUKA
Kaimu
Mkurugenzi, Kurugenzi ya Mawasiliano Ofisi ya Rais Ikulu, Gerson
Msigwa, alisema kuyumba kiuchumi kwa hoteli nchini kutokana na agizo la
Rais Magufuli si kazi ya serikali na wala agizo hilo haliwezi
kubadilishwa.
Alisema
Rais Magufuli alitoa agizo hilo kwa dhumuni la kupunguza matumizi
yasiyo ya lazima kwa serikali na kuwataka Watanzania wote wapenda
maendeleo wamuunge mkono katika suala hilo.
“Wizara
zilikuwa zinatumia pesa nyingi sana kukodi kumbi kwa saa kadhaa wakati
kuna kumbi katika wizara zao. Sasa kuyumba kiuchumi au kukosa wateja
katika hoteli hiyo si kazi ya Ikulu,” alisema Msigwa.
Alisema
hoteli zinapaswa kuwa wabunifu wa kupata fedha zaidi na si kutegemea
wizara au taasisi kwenda kufanya mikutano katika hoteli zao.
Imeandaliwa na Gwamaka Alipipi, Fredy Azzah, Elizabeth Zaya na Efracia Massawe.
CHANZO: NIPASHE
