ASKARI AMBAYE NI JAMBAZI AUWA KWA KUPIGWA RISASI



Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari.
Askari polisi Konstebo Norbert Chacha (25) ameuwawa kwa kupigwa risasi kifuani na mgongoni wakati akifanya ujambazi.

Mauaji ya askari huyo yalitokea usiku wa kuamkia juzi usiku wa manane katika kijiji cha Ibindi, wilayani Mlele, akiwa na watu wengine ambao walikuwa wamekwenda kufanya ujambazi kwenye nyumba ya mfanyabiashara wa madini ya dhahabu kijijini hapo.

Diwani wa Kata ya Machimboni, Raphael Kalinga, aliwaambia waandishi wa habari kuwa askari huyo akiwa na kundi la majambazi wenzake, ambao idadi yao haikufahamika, walifika kijijini hapo kwa lengo la kumvumia na kumpora mfanyabiashara huyo, Daniel John.

Alisema baada ya kufika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo, walivunja mlango wa mbele, wakati mfanyabiashara huyo akiwa amelala.

Majambazi hayo, alisema baada ya kuvunja mlango, waliingia ndani na mfanyabiashara aliwauliza ni kinanani na ndipo walipomwamuru asipige kelele vinginevyo watamuua.

Kalinga ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, alisema kutokana na amri hiyo, John alichukua bunduki yake ya shotgun na kufyatua risasi ambayo ilimpiga askari huyo kifuani na mgongoni na kufa hapo hapo.

Alisema majambazi wenzake ambao walikuwa na mapanga na shoka baada ya kuona mwenzao kapigwa risasi na kufa waliamua kumbeba marehemu na kwenda kumtupa kichani umbali wa mita 200 kutoka kwenye eneo la tukio na kisha walitokomea kusiko julikana.

Wakazi wa Kijiji hicho walifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo na kukuta michirizi ya damu na ndipo walipoamua kuifuata ilikokuwa inaelekea.

Alisema wanakijiji waliendelea kuifuata michirizi hiyo na walipofika umbali wa mita 200 kutoka nyumbani kwa John, waliuona mwili wa askari polisi huyo ambaye alikuwa amefariki dunia kutoa taarifa polisi wilaya ya Mpanda.

Polisi walifika kwenye eneo hilo baada ya muda mfupi na ndipo walipomtambua marehemu kuwa ni askari polisi wa kituo cha cha wilaya ya Mpanda .

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, amethibitisha kuuwawa kwa askari huyo kuwa alipigwa risasi akiwa katika harakati za kufanya ujambazi na kupora .

Alisema mwili wa marehemu bado umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda .

Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa mkoa wa Katavi waliokuwa wakiwatuhumu baadhi ya askari polisi kuhusika katika matukio ya ujambazi na uporaji mkoani hapa.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.