CUF Yasema Ina Imani na Magufuli

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimewataka Wazanzibari kuwa watulivu na kumpa nafasi zaidi Rais John Magufuli kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa Zanzibar, ambao umetokana na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu. Alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana kuhusu hali ya kisiasa visiwani hapa.
Jussa alitumia nafasi hiyo kujibu baadhi ya taarifa zilizotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu ambayo inatokana na kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kilichofanyika mwishoni mwa wiki.
Jussa alisema vikao vya kusaka suluhu ya kudumu Zanzibar, ambayo inatokana na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, vinaendelea chini ya viongozi, wakiwemo marais wastaafu. Alisema vikao hivyo ni kwa mujibu wa taarifa ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliyoitoa Ikulu mjini Dar es Salaam.
Taarifa kamili itatolewa kwa wananchi mara vikao hivyo vitakapomaliza kazi zake. Jussa alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake binafsi kwa kukutana na kamati ya viongozi ikiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwa nyakati tofauti.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.