WABUNGE WAGOMEA MILIONI 90 ZA MASHANGINGI,WATAKA ZIONGEZWE
Picha hii kutoka Bungeni juzi Rais magufuli aluipolihutubia Bunge Wakati Serikali ikihaha kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake, wabunge wameingia kwenye mvutano na ofisi ya Bunge kuhusu fedha ambazo watunga sheria hao wanastahili kupewa kwa ajili ya kununulia magari yao.
Mwaka 2010, wabunge walilipwa Sh90 milioni kwa ajili ya ununuzi wa magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser (hardtop), ambayo ni vitendea kazi vyao. Wabunge hutakiwa kulipa nusu ya fedha hizo wkati nyingine ni mchango wa Serikali.
Lakini wakati gharama za maisha zikipanda huku thamani ya Shilingi ikiporomoka kulinganisha na Dola ya Marekani na hivyo kusababisha bidhaa kupanda bei, wabunge wamekataa kulipwa kiasi hicho cha fedha mwaka huu na badala yake wanataka walipwe kulingana na bei ya sokoni ya magari aina hiyo.
Kwa mujibu wa habari ambazo Mwananchi imezipata, wabunge wanataka walipwe Sh130 milioni ambazo wanasema ni bei ya magari hayo kwa sasa baada ya kupanda bei.
Wakizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina, baadhi ya wabunge walisema mara baada ya kujisajili bungeni kwa ajili ya uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja, katibu wa chombo hicho, Dk Thomas Kashililah alifanya kikao na wabunge wote ili kuwapa taratibu lakini pia kuwafahamisha stahili wanazopaswa kupata kama wabunge.
“Katibu alitujulisha kuwa tunapaswa kulipwa kiasi cha Sh300,000 kwa siku za posho, lakini pia tutapewa Sh90 milioni kwa ajili ya mkopo wa gari ambao nusu hutolewa na ofisi ya Bunge na kiasi kilichobaki tunapaswa kulipa wenyewe,” alisema mmoja wa wabunge hao.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, suala hilo liliibua mjadala na kusababisha wabunge kuhoji iweje kiwango hicho kitumike katika Bunge la Kumi na Moja, miaka mitano baada ya wabunge wa Bunge la 10 kupewa kiasi hicho.
“Unajua magari tunayotakiwa kununua ni Toyota Land Cruiser Hardtop, na ukweli sasa thamani ya magari hayo imepanda sana huwezi kuifananisha na mwaka 2010 wakati wa Bunge la 10,” alisema mbunge mmoja.
Wabunge hao walitaka walipwe kiasi cha Sh130 milioni kwa madai kuwa ndiyo bei ya sokoni ya magari aina hiyo.
Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Anatropia Theonest alikanusha habari hizo akisema hawajakataa fedha hizo, lakini walisema thamani ya Dola imepanda hivyo kusababisha thamani ya magari hayo kupanda pia.
“Hakuna asiyejua kwamba thamani ya Dola imepanda na kwa kawaida kila Bunge kunakuwa na ongezeko la Sh30 milioni. Mfano Bunge la Tisa walipewa Sh60milioni la 10 wakapewa Sh90milioni, hivyo ilipaswa sasa iwe Sh 120mililioni ili kuendana na soko,” alisema mbunge huyo.
Alisema baada ya mazunguzo hayo ofisi ya Bunge iliahidi kulifanyia utafiti suala hilo na kwamba ingewajibu.
Lakini, Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu alisema wabunge wanapaswa kufahamu wapo kwa ajili ya wananchi na si kujilimbikizia mali.
“Kwa mfano mimi siwezi kuchukua fedha za posho kwa ajili ya kikao. Nimepanga kumuandikia barua Spika juu ya uamuzi wangu. Mshahara wangu unanitosha kabisa,” alisema Kingu ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga kabla ya kutolewa katika nafasi hiyo na kugeukia ubunge.
Akizungumzia sakata hilo, katibu wa Bunge alisema masharti na vigezo vilivyotumika mwaka 2010, ndivyo vinavyoendelea kutumika katika Bunge hili, na hivyo hakuna kilichobadilika.
Dk Kashililah alisema fedha za magari hayo hutolewa na Wizara ya Fedha kama mkopo na wabunge wataulipia huku kiasi kingine wakipewa kama ruzuku ya kununulia magari.
Hata hivyo hakutaka kuzungumzia kiwango halisi cha fedha zinazotolewa kwa wabunge hao.
Awali naibu katibu wa Bunge, John Joel alisema jukumu la ununuzi wa magari ya wabunge, lipo chini ya Serikali na siyo ofisi yake hivyo ni bora wangeulizwa wenye jukumu hilo.
“Tunachofamu sisi mbunge anatakiwa apewe vitendea kazi likiwemo gari, lakini wanaohusika na hilo ni Serikali,” alisema.
“Sisi huwa tunawahudumia jimbo allowance (posho) kwa ajili ya kuhudumia ofisi ya mbunge na kununua mafuta ya gari,” alisema Joel bila kutaja kiwango cha posho hiyo.
Alisema ofisi ya Bunge hushauriana na Serikali namna ya kutoa huduma kwa wabunge na kwamba kwa jinsi anavyofahamu, mpaka jana watunga sheria hao walikuwa hawajapewa fedha yoyote ya kununua magari kwa awamu hii, hivyo wanasubiri utaratibu.
Wakati Joel akisema Serikali ndiyo inahusika, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue aliurudisha mpira kwenye ofisi hiyo ya Bunge, akisema uongozi wa chombo hicho ndio uulizwe.
Katika kukusanya fedha za kuwezesha kutekeleza mipango ya Serikali na ahadi alizotoa wakati wa kampeni, Rais John Maguguli alitangaza hatua mbalimbali za kudhibiti matumizi, na akawaeleza wabunge mwishoni mwa wiki kuwa hataweza kufanikiwa iwapo hatapata ushirikiano wao.
Katika kuonyesha kuwa anatoa kauli thabiti, Dk Magufuli aliagiza fedha ambazo zilichangwa na taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya hafla za kuwapongeza wabunge, zielekezwe kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Tayari Rais ameshafuta safari za nje isipokuwa kwa kibali cha Ikulu baada ya mtu anayetaka kusafiri kutimiza masharti kadhaa, likiwamo linalomtaka aeleze faida ya safari yake na kama iwapo hatasafiri, nchi itaathirika vipi.
Imeandikwa na Tausi Mbowe, Nuzulack Dausen na Florence Majani