SITTA KUWANIA NAFASI YA SPIKA KATIKA SERIKALI YA MAGUFULI
WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta ametangaza kuwa atawania nafasi ya
Spika ili kuliongoza Bunge la 11. Sitta aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la
Tisa amekuwa kada wa kwanza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitosa
katika mchuano wa kuwania nafasi hiyo nyeti wakati huu ambao Bunge
limevitaka vyama vya siasa viwe tayari kwa ajili ya kupeleka majina ya
wateule wao wa nafasi hiyo mara itakapotangazwa kuwa wazi.
Msemaji wa Spika huyo mstaafu, John Dotto alisema jana Dar es Salaam
kuwa Sitta amemua kuwania nafasi hiyo kutokana na uwezo na uzoefu
alionao wa kuendesha Bunge. Alisema Sitta anaamini kuwa uwezo wake
aliouonesha katika kuendesha Bunge la Tisa akitumia kaulimbiu yake ya
‘Spika wa Kasi na Viwango’ itamfanya aendane na kasi ya utendaji wa Rais
Mteule, Dk John Magufuli.
Sitta alijizolea sifa wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa kuanzia
mwaka 2005 hadi 2010, ikiwamo Bunge hilo kufanyia marekebisho ya kanuni
mbalimbali zilizolifanya liwe na makali na kuibua kashfa nzito ikiwamo
ya Richmond ambayo ilisababisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu na
alilirejeshea makali Bunge.
Tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano limetangaza kuanza kwa mchakato
wa kumpata Spika mpya wa Bunge, atakayerithi mikoba ya Spika Anne
Makinda. Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel akizungumza na vyombo vya
habari Dar es Salaam mapema wiki hii alisema kuwa mgombea wa nafasi ya
Spika, anaweza kuwa Mbunge au mwanachama yeyote wa chama kwa masharti
kwamba kama si Mbunge, jina lake lazima liwasilishwe kwanza Tume ya
Taifa ya Uchaguzi siku tano kabla ya uchaguzi kujiridhisha kuwa mgombea
huyo ana sifa za kuwa Mbunge.
Bunge hilo la Tisa lilipata ufanisi na mafanikio kadhaa kutokana na
ubunifu na ujasiri wa baadhi ya wabunge wakiongozwa na utayari wa Sitta
ambaye wakati akishika nafasi hiyo aliahidi kuwa ‘spika wa kasi na
viwango.’
Mafanikio yaliyopatikana katika Bunge hilo ni pamoja na kutungwa kwa
Kanuni mpya za Bunge za mwaka 2007, ambazo zimeelezwa kuwa zilisaidia
kwa kiasi kikubwa kuliwezesha lifanye kazi kwa ufanisi kama vile kuondoa
ukiritimba wa serikali kuwa ndiyo pekee inayoweza kupeleka muswada
bungeni.
Kanuni hizo mpya za mwaka 2007 ambazo zilitokana na kufanyia
marekebisho makubwa kanuni za Bunge za mwaka 2004, zilitoa mamlaka kwa
kamati za kudumu za Bunge kuwa na uwezo wa kupeleka mswada kwa ajili ya
kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwa sheria.