'Mchagueni Lema tukapiganie Tume Huru ya Uchaguzi'


Mbunge mteule wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga.
Mbunge mteule wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga (Chadema), amewaomba wakazi wa Jiji la Arusha, kumchagua Godbless Lema kuwa mbunge wao ili wakapiganie kupatikana kwa katiba bora na zaidi Tume Huru ya Uchaguzi.
 
Kalanga aliyasema hayo juzi katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za mgombea huyo uliofanyika eneo la Soko Kuu jijini hapa.
 
“Arusha msifanye makosa, mchagueni Lema tukapiganie Katiba bora ya Tanzania na Tume Huru ya Uchaguzi,” alisema na kuongeza:
 
“Tusiwe wanyonge watu wa Arusha, unachukuaje kura ya Chadema na kuwapa watu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili watoto wako wafe njaa, hata kama anayegombea CCM ni shemeji yako usimpe kura yako,” alisema.
 
“Haiwezekani mkawapigia kura madiwani 24 wa Chadema dhidi ya mmoja wa CCM jimboni hapa, halafu mkashindwa kumpigia kura mgombea ubunge wa chama chenu,” alisema.
 
Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya wakazi wa hapa kujiandaa kupiga kura kwa misingi ya ukabila akisema uchaguzi wa mbunge utakaofanyika Desemba 13, mwaka huu sio wa kumchagua kiongozi wa kimila.
 
“Hatuchaguzi kiongozi wa mila hapa, tuwakatae wanaofanya ubaguzi,” alisema.
 
Kwa upande wake, Mbunge mteule wa Jimbo la Simanjiro, James Ole Millya (Chadema), alimtaka Rais Dk. John Magufuli kujenga mfumo wa kutatua ufumbuzi wa kero za wananchi badala ya yeye kupita kila kona kukagua shughuli za utendaji.
 
“Magufuli ameanza kwa kufukuza huyu na kumsimamisha yule…tunataka akae ofisini na kujenga mfumo mzuri wa utendaji serikalini. Hawezi kutembelea kila sehemu mwenyewe,” alisema.
 
Aliwapongeza watu wa mikoa ya Kaskazini kwa kutochezea kura zao kama ilivyokuwa maeneo mengine.
Alisema uchaguzi mkuu uliopita uliandaliwa kwa muda mrefu kuwezesha wagombea wa CCM kushinda, hivyo kuufanya kuwa kiini macho. Akizungumza katika mkutano huo, Lema alisema hatakubali kuibiwa kura zake na kupewa mgombea mwingine.
 
“Wamenyang’anywa ubunge wagombea wengi wa Chadema, lakini mimi sitakubali kudhulumiwa hilo kabisa,” alisema.
 
Aidha, alitoa angalizo kwa polisi mkoani hapa kutenda haki, badala ya kufanya kazi za ukada wa CCM.
 
Alisema kumekuwa na tabia ya polisi kujiingiza katika masuala ya siasa huku akidai kuwa wamekuwa wakitoa upendeleo kwa CCM.
CHANZO: NIPASHE
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.