MATOLA KUFUNDISHA LIGI DARAJA LA KWANZA
Baada ya Selemani Matola kujiuzulu nafasi yake kama kocha msaidizi wa Simba kwa kinachodaiwa kutoelewana na kocha mkuu wa timu hiyo Dylan Kerr, hatimaye kocha Selemani Matola ameingia mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha timu ya Geita Gold SC inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania bara.
Akizungumza na mtandao huu Matola amesema, baada ya kuachana na Simba alipata offer kutoka timu nyingi ila offer ya Geita Gold SC ilikuwa nzuri zaidi.
“Kwanza nikueleze nilipata offer nyingi sana kabla ya kuja Geita lakini niliweza kuangalia sera za timu zinakwenda vipi, baada ya kuongea na uongozi wa Geita hasa mwenyekiti Bw. Salum kiukweli niliona ni watu wenye mwelekeo mzuri katika hali ya kupandisha timu. Kwahiyo siku zote mwalimu unategemea kwenda sehemu ambayo unaona inamwelekeo mzuri”.
“Mimi nimeichagua Geita kwasababu ni timu inayoonekana inamalengo ya baadae, nitajitahidi kwa uwezo wangu kwa kushirikiana na viongozi wa hapa tufanye kile kinachowezekana kuhakikisha timu inapanda ligi kuu”.
Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Geita Bw. Salumu Kulunge amesema wameamua kumtafuta Matola kwasababu anauwezo mkubwa wa kazi hiyo na wanaamini ataipandisha timu hiyo kucheza ligi kuu msimu ujao.
“Kuna mambo mengi ambayo yametokea na mpaka tumeamua kumleta yeye kwakweli kuna mapungufu mengi ambayo kama viongozi tumeyaona ndiyomaana tukaona ni vizuri kukawa na kocha ambaye tunaamini kabisa uwezo na jitihada zake za ushindani zinaweza zikatupeleka pale sisi tunapohitaji na hiyo ndiyo sababu kubwa iliyotufanya sisi tushawishike kumchukua Matola”.
“Tunamfahamu vizuri sana baadhi yetu tumechezanaye mpira lakini baada ya hapo mwenzetu aliendelea katika ngazi ya ukocha na sisi tukajiendeleza katika mambo mengine”.
Kwa upande wake kocha msaidizi wa timu hiyo Teru Yusuf Mpeka amesema anafarijika Matola kujiunga na Geita huku katibu mku wa timu hiyo Mnenge Suluja akisema wameamua kumuacha kocha Kim Kristopher kwakua hakuwa mkweli kipindi wanaingia mkataba kuinoa kikosi hicho.
“Tumefarijika sana kwa ujio wa kocha Selemani Matola katika timu yetu kuja kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi la timu yetu nafikiri itakuwa chachu ya maendeleo kwenye timu yetu, itabadilika sana kutoka hapa ilipo”.