MANENO YA MWAMBUSI DHIDI YA MECHI YA TAIFA STARS NA NIGERIA YALETA FARAJA

Kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi
Kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
SIKU chache kabla ya kuwavaa Algeria ‘desert fox’, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inapaswa kutambua ugumu wa mchezo huo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa hatua ya makundi kufuzu kombe la dunia 2018, fainali ambazo zitafanyika nchini Urusi.
Stars imefanikiwa kufuzu kwa hatua ya pili ya mtoano-Kanda ya Afrika baada ya kuwaondoa majirani zetu wa Kusini, timu ya taifa ya Malawi. Mechi ya Jumamosi hii itakuwa dhidi ya ‘Mweha wa Jangwani’ ambao ni miongoni mwa timu mbili kutoka barani Afrika ambazo zilifanikiwa kufika hatua ya 16 katika fainali za ‘Brazuca 2014’.
Ili kufuzu kwa hatua ya mwisho ya mtoano kabla ya hatua ya makundi Stars inapaswa kucheza kwa heshima.
“Ni mchezo mgumu, lakini maandalizi, nia na kujitoa kwa wachezaji hakuna lisilowezekana” anasema kocha msaidi wa mabingwa wa ligi kuu bara, Juma Mwambusi wakati nilipofanya nae mahojiano mafupi siku ya Jumanne wiki hii.
Stars imekuwa na kambi ya maandalizi kwa siku 10 nchini Afrika Kusini chini ya wakufunzi, Charles Mkwassa, Hemed Morocco na mshauri mkuu, Abdallah Kibadeni. Ilifungwa 2-0 na timu ya taifa ya vijana ‘U23’ ya Afrika Kusini siku ya Jumanne hii katika mchezo wa kujipima uwezo.
Licha ya mkufunzi mkuu, Mkwasa kutetea kipigo hicho kwa madai kuwa, wachezaji wake walicheza kwa tahadhari ya kuogopa kuumia ukweli wanapaswa kuwa makini zaidi katika mchezo huo. Algeria ilitolewa na Ujerumani katika hatua 16 bora katika michuano ya Brazil mwaka uliopita ni timu namba moja kwa ubora barani Afrika hivi sasa. Itashangaza wengi ikiwa timu hiyo itatolewa na Tanzania lakini katika mpira wa miguu kila kitu kinawezekana.
“Walimu wanajua nini cha kufanya. Jambo muhimu katika dakika 15 za mwanzo ni kuwa waangalifu, nidhamu ya hali ya juu ya kimchezo kwa wachezaji wetu. Tupo nyumbani, tusikubali kufungwa goli la mapema”, anasema Mwambusi kocha wa zamani wa Tanzania Prisons, Moro United, Polisi Dodoma na Mbeya City FC.
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.