MAJANGA TENA>>>>ASIMILIA 82 YA WANAFUNZI WAKOSA MIKOPO 2015/16
Zaidi
ya wanafundi 50,000 watashindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu
kutokana na kushindwa kupata mikopo kutoka katika Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu (HESLB).
Hayo
yamebainika ikiwa ni siku tatu tangu HESLB kutoa majina ya wanafunzi
waliofanikiwa kupata mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016, huku idadi
kubwa ikiwa haimo katika majina hayo.
Katika
mwaka huu wa masomo bodi ya mikopo imeweza kuwapatia mikopo wanafunzi
12,000 pekee sawa na 17.1% ya waombaji zaidi ya 70,000, hivyo kufanya
idadi ya wanafunzi waliokosa mikopo kufikia asilimia 82.9 ya waombaji
wote.
Wanafunzi
waliokosa mikopo ya kuwawezesha kujiunga na elimu ya juu na hivyo
wazazi wao kutakiwa kugharamia elimu hiyo wameelezea kusikitishwa na
hali hiyo huku wakiitaka serikali kuwaangalia kwa jicho la kipekee kwani
hawana uwezo wa kuanza masomo pasipo kufadhiliwa na serikali.
Wanafunzi
hao walionekana kukata tamaa ya kutimiza ndoto yao ya kujiunga na elimu
ya chuo kikuu, wamefika makao makuu ya bodi hiyo huku wakiongozana na
baadhi ya viongozi wa serikali ya wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) kutaka kujua hatima yao.
“Nimetokea
Tabora, wazazi wangu walinipa Sh. 100,000 ya kutumia wakiamini tunapewa
mikopo na serikali, lakini tumenyimwa na hatujui hatima yetu,
nimebakiwa na Sh. 6,000, naomba serikali ituhurumie, isikie kilio chetu
hatustahili kuteseka hivi,” ameeleza Abdul Omary mwanafunzi mteule UDSM.
Fatuma
Bakari, mwanafunzi mwingine kutoka UDSM, amesema: “Siwezi kujiunga na
Chuo bila mkopo, tumefika hapa ili kuomba bodi ya mikopo itusaidie
hatuna tumaini lolote zaidi ya kuomba Mungu atusaidie tuweze kupata
mikopo na kuanza masomo.”
Waziri
wa Mikopo serikali ya wanafunzi (Daruso), Shitindi Venance ameeleza
kutokukubaliana na majibu waliyopewa na uongozi wa juu wa bodi ya mikopo
kwani yanakatisha tamaa na kuzima ndoto za wanafunzi wa masikini kusoma
chuo kikuu.
“Hapa
UDSM ni wanafunzi 600 tu waliopata mikopo kati ya wanafunzi 7,000
waliopangiwa kuanza masomo, hili ni janga kubwa kwa watoto wa masikini
kwani hawawezi kujisajili chuoni wala kupata makazi katika mabweni mpaka
walipe ada na wengi wametoka mikoani.
“Tunachukua
hatua moja mbele na kuamua kulifuatilia suala hili kwa katibu mkuu wa
wizara ya elimu na katibu mkuu wa wizara ya fedha kwa sababu bodi bado
wanasisitiza tuwe na subira ilihali muda umeenda na wanafunzi
wanateseka” ameeleza Shitindi.
Mkurugenzi
wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole amewaambia
wanahabari waliofika ofisini kwake kuwa bodi haistahili kulaumiwa kwani
serikali kupitia wizara ya fedha na wizara ya elimu ndio yenye uwezo wa
kutenga kiasi cha fedha kulingana na mahitaji ya wakati husika.
“Lengo
la bodi ya mikopo ni kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kusoma kwa
ufadhili wa serikali na wala sio kuwakwamisha, tunaendelea kujadiliana
na serikali kuona kama itatuongeza fedha ili tuweze kutoa awamu ya pili
ya majina ya wanafunzi waliopata mikopo, tunawaomba wanafunzi wavute
subira,” anaeleza Ngole
Hata
hivyo Ngole amesema hawezi kusema lini watatangaza majina ya awamu ya
pili kwani hilo linategemea ni lini serikali itatoa fedha kwa ajili ya
wanafunzi wa awam ya pili.
Katika
mwaka uliopita wa masomo 2014/2015 serikali ilitoa mikopo kwa wanafunzi
30,000 sawa na 51.7% ya waombaji wote 58,000 na hivyo kufanya waliokosa
mikopo kuwa wanafunzi 28,000 sawa na 49% pekee tofauti na mwaka huu
ambapo waliokosa wamefikia asilimia 82.9