MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI MWAKA 2015 KUFANYIKA KITAIFA DESEMBA MOSI MKOANI SINGIDA
Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk.Fatma Mrisho (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani mwaka 2015 yatakayofanyika kitaifa Desemba Mosi mkoani Singida. Kulia ni Mkurugenzi wa Habari na Uraghibishi.
Na Dotto Mwaibale
MAAMBUKIZI
ya virusi vya Ukimwi nchini yameongezeka kwenye kundi la vijana wenye
umri wa miaka kati ya 19 mpaka 24 tofauti na ilivyokuwa miaka minne
iliyopita, ambako kundi lililokuwa limeathiriwa zaidi lilikuwa miaka
kati ya 25 mpaka 34, imeelezwa.Pia licha ya kwamba kiwango cha maambukizi mapya ya virusi hivyo nchini kimeshuka kutoka asilimia 7 mwaka 2004 mpaka kufikia asilimia 5.3 mwaka huu, takwimu za baadhi ya mikoa ikiwemo Singida, Kigoma, Arusha, Mtwara, Kilimanjaro na Kagera zimeonekana kuongezeka.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani kwa mwaka huu, Dk. Fatma Mrisho, alisema kazi kwa ujumla kazi kubwa imefanyika.
Alisema ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita, maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi yamepungua kwenye maeneo mengi ya nchi kutokana na jitihada za serikali, wadau na wananchi kwa ujumla.
Dk. Mrisho alisema licha ya mikoa kadhaa kuendelea kuandamwa na maambukizi hayo, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo maendeleo na mwingiliano wa watu, mikoa ya Tanga na Manyara ndiyo yenye takwimu chache za maambukizi zikiwa na asilimia 4 pekee.