Lowassa chanzo cha Mwanri, Anne Kilango kuanguka - CCM
Mh. Edward Lowassa.
Lema amedai kuangushwa kwa mawaziri wawili wa serikali iliyopita,
Aggrey Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Anne Kilango Malecela
(Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Dk. Cyril Chami,
kulitokana na ushawishi mkubwa wa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema,
Edward Lowassa.
Lema aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Nipashe, kuhusiana
na tathimini yao waliyoifanya Novemba 7, mwaka huu baada ya kupitia
zoezi zima la uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema Lowassa ndiye aliyeisaidia Chadema kuwapokonya majimbo hayo
kutokana na kuungwa mkono na wananchi wengi wakiwamo pia baadhi ya
makada wa CCM ambao hawakufurahishwa na kitendo cha Kamati Kuu ya chama
hicho kuliengua jina lake wakati wa mchakato wa uteuzi ndani ya chama
hicho.
“Chadema imefanikiwa kuchukua majimbo ya CCM kutokana na mkakati wa
Lowassa pamoja na kuhama kwake, kitu ambacho kilitengeneza mpasuko
ulioiua CCM na wagombea wake,” alisema.
Alidai kulitokea usaliti ndani ya CCM kwa madai kulikuwa na kundi
ambalo lilikuwa likiendelea kushiriki vikao vya ndani huku likikerwa na
kuondoka kwa Lowassa jambo ambalo lilisababisha chama hicho kushindwa
katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Aidha, akizungumzia mkakati wa
CCM kuyarejesha mikononi mwake majimbo ya Moshi Mjini na Rombo, Lema
alidai kuwa sababu ya kushindwa kwao ni kutokana na wagombea wa nafasi
za ubunge kupitia chama hicho kupora mamlaka ya viongozi wa wilaya.
“Wagombea ubunge katika majimbo haya mawili walikuwa na nguvu zaidi
katika chama, atakalolisema yeye na atakalopanga ndilo atakalolisimamia
lifanyike. Ukweli ni kwamba viongozi wa wilaya nao waliwaogopa, huku
kampeni zao zikikwepa kabisa kuwashirikisha viongozi wa chama ngazi za
matawi na kata” alisema Lema.
Alisema pamoja na kwamba CCM kilianzisha vikosi kazi maalum kwa
ajili ya kutafuta kura, lakini katika hali ya kushangaza wagombea wao wa
ubunge katika majimbo yote tisa ya Mkoa wa Kilimanjaro, walijiweka
kando kuwatumia viongozi wa matawi na ngazi ya kata.
Sababu nyingine ya kupoteza viti vingi vya udiwani alisema ni
wagombea wao kujiaminisha kwamba CCM ingewaletea fedha nyingi kwa ajili
ya kampeni huku wengine wakiamini wangesaidiwa na wagombea ubunge ambao
waliamini walikuwa na fedha nyingi kuwashinda wagombea wa vyama vya
upinzani.
CHANZO:
NIPASHE