Kikwete Aaga Kwa Kusamehe Wafungwa 4,160
RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,160 katika kuaga na kukabidhi madaraka ya Serikali kwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.
Dk
Magufuli aliapishwa jana kuwa Rais wa Tano wa Tanzania katika sherehe
zilizofana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Kikwete akimaliza
miaka yake 10 ya kuongoza nchi kama ilivyoelekezwa na Katiba.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam, kati ya
wafungwa hao, wafungwa 867 wataachiwa huru na wafungwa 3,293
watapunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya
vifungo vyao vilivyobaki.
“Ni
mategemeo ya Serikali kwamba wafungwa watakaoachiwa huru watarejea
katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa na
watajiepusha na utendaji makosa ili wasirejee tena gerezani,”alisema Chikawe katika taarifa hiyo.
Chikawe
aliwataja walionufaika na msamaha huo kuwa ni wafungwa wote wapunguziwe
moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa
chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa
wafungwa walioorodheshwa katika ibara ya 1 (i-xix).
Aliwataja
wengine kuwa ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua
kikuu, saratani ambao wako kwenye hatua ya mwisho ambao watathibitishwa
na waganga chini ya Mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Pia
wazee wenye umri zaidi ya miaka 70, wafungwa wa kike walioingia na
mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya na
walemavu wa mwili na akili na ulemavu huo uthibitishwe na jopo la
waganga.
Kwa
mujibu wa Chikawe, msamaha hautawahusu wafungwa wenye adhabu za
kunyongwa, waliohukumiwa kunyongwa na adhabu hiyo baadaye kubadilishwa
kuwa kifungo cha maishaau kifungo gerezani.
Wengine
ni wafungwa waliotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji na utumiaji
wa dawa za kulevya, makosa yanayohusu uombaji, upokeaji na utoaji
rushwa, unyang’anyi na kujaribu kutenda makosa hayo, kubaka, kulawiti au
kujaribu kutenda makosa hayo.
Aidha,
makosa mengine ambayo vifungo vyake haviko kwenye msamaha huo ni makosa
ya kuwapa mimba wanafunzi, wizi wa magari, pikipiki au kujaribu kutenda
makosa hayo, matumizi mabaya ya madaraka, waliowahi kupunguziwa vifungo
na Rais.
“Wengine
ni waliopatikana na hatia kwa kuwazuia watoto kupata masomo, utekaji
watoto, usafirishaji binadamu, ukatili dhidi ya albino, usafirishaji
nyara za Serikali na ujangili,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mengine
ni wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi na ubadhirifu wa fedha za
Serikali, kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali na
wafungwa wanaotumikia vifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole Sheria
Namba 25 ya Mwaka 1994 ya Sheria ya Huduma kwa Jamii Namba 6 ya Mwaka
2002.