Balozi Seif afunguka hali ya Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema suala la kurudiwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar halina mjadala baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, kuhujumiwa visiwani humo.

Balozi Seif ametoa msimamo huo wa serikali baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuweka msimamo kuwa haukubaliani na kitendo cha mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), kufuta matokeo na kuamua kurudiwa upya.

Akizungumza na Nipashe Jumapili Mjini Zanzibar Balozi Seif, alisema kuwa Serikali imeridhia uamuzi wa Zec kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

“Serikali tumeridhia uamuzi wa tume wa kufuta matokeo baada ya uchaguzi wa awali kuhujumiwa na sasa tunasubiri tarehe ya kufanyika uchaguzi kutangazwa na tume ya uchaguzi ya Zanzibar,”alisisitiza Balozi Seif.

Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, matokeo yaliyo futwa yalikuwa yametawaliwa na vitendo vya udanganyifu na kupoteza sifa na viwango vya kuwa uchaguzi huru na wa haki.

Hata hivyo, alisema ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya waangalizi wa nje na wa ndani kushindwa kuyazingatia katika ripoti zao matatizo yote yaliyojitokeza katika uchaguzi huo.

Balozi Seif alisema kwamba serikali imo katika matayarisho ya kuandaa gharama ili kuhakikisha Wananchi wanapata haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka kidemokrasia.

Hata hivyo, alisema suala la vyama vya siasa kushiriki au kutokushiriki ni hiyari yao, muhimu wananchi wapate haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi kwa njia halali bila ya kufanyika udanganyifu.

Balozi Seif alisema, SMZ itahakikisha uchaguzi huo unafanyika haraka huku serikali ikiendelea kufanya uchunguzi dhidi ya watu waliohusika na kuhujumu uchaguzi wakiwamo baadhi ya watendaji visiwani hapo.

"Kila mtu ambaye hataguswa na ushahidi lazima afikishwe katika mkono wa sheria,” alisema Balozi Seif.

Balozi Seif alisema hali ya Zanzibar imerejea kama kawaida na wananchi wa Unguja na Pemba wanaendelea na shughuli zao na kuwataka wawekezaji kuondoa hofu.

Aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuimarisha doria ili kuendeleza kulinda hali ya amani na usalama wa raia na mali zao kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi huo.

Kwa upande wake, Kiongozi Mwadamizi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Janet Fussi, alisema visiwani humo jana, hawakubaliani na uamuzi wa kufuta matokeo na kurejewa kwa uchaguzi huo.

Fussi ambaye pia ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alisema uchaguzi uliofutwa ulikuwa huru na wa haki na kutaka matokeo yaendelee kuhakikiwa katika majimbo 23 yaliobakia na mshindi atangazwe.

“Ufumnbuzi pekee wa mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar, mwenyekiti wa tume arudi kazini akamilishe kazi aliyopewa ya kuhakiki matokeo na kumtangaza mshindi wa urais wa Zanzibar,” alisema.

Alisema haiwezekani Mwenyekiti wa Zec afute matokeo ya uchaguzi kibabe na kuitisha uchaguzi mpya baada ya kuona mwelekeo mbaya dhidi ya CCM, katika uchaguzi huo.

Alisema kinachooneka CCM bado hawakubali mabadiliko ya kiutawala kupatikana kwa njia ya demokrasia ndiyo maana wanashindwa kuheshimu maamuzi ya wananchi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, alitoa sababu tisa zilizosabisha kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo na kuamua urudiwe, ikiwemo kura katika vituo kupita idadi ya watu waliosajiliwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Sababu nyigine ni kuhamishwa kwa masanduku ya kura na kuhesabiwa nje ya vituo kinyume na taratibu, kupigwa mawakala na kutolewa nje ya vituo, vijana kuvamia vituo na kuanza kupiga watu na kuzuwia watu wasiokua wa vyama vyao kufika katika vituo vya kupiga kura na kupiga kura.

Aidha, alisema walipokea malalamiko mengi kutoka vyama mbalimbali yanayoashiria kutoridhika na mchakato wa mzima wa upigaji kura, kuhesabu na kutoa matokeo ya uchaguzi huo, pamoja na namba za fomu za matokeo ya vituo vingi vya Pemba kuonekana kufutwa na kuandikwa upya.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Theme images by hanoded. Powered by Blogger.