WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI JIJINI MWANZA
Rashid Mkumba Hamis ambaye ni mmoja wa majeruhi aliyevunjika mguu.
Majeruhi katika tukio hilo wakihojiwa na wanahabari (hawapo pichani).
Askari wakiendelea kuwaokoa wananchi katika jengo lililoanguka jijini Mwanza.(P.T)
Vikosi vya uokoaji vikitoa msaada eneo la tukio.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Kunisaga akiongea na wanahabari baada ya ajali hiyo.
Eneo la msingi uliokuwa unajengwa na kuangukiwa na ukuta.
Wananchi wakishuhudia tukio hilo.
Vijana wakijaribu kuokoa baadhi ya mali zilizofukiwa na kifusi hicho.
Picha / Habari: Johnson James, GPL / Mwanza
Watu
watano katika Wilaya ya Nyamagana jijini hapa wamenusurika kifo baada ya
kuangukiwa na kifusi wakati wakiwa kwenye maandalizi ya kujenga jengo
lililotegemewa kuwa na ghorofa saba, eneo la Nyerere Road, leo majira ya
saa sita mchana.
Akizungumza
na waandishi wa habari eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,
Baraka Kunisaga amesema kuwa amesikitishwa na tukio hilo ambapo watu hao
wameangukiwa na ukuta wakati wakijenga msingi wa jengo hilo na hii ni
kutokana na kuwa na wakandarasi ambao hawajengi majengo kwa kiwango
kinachotakiwa.
Katika
hatua nyingine, Kunisaga amesema kuwa hali ya Watanzania kuwa wanapoteza
uhai wao kila kukicha kutokana na kuangukiwa na vifusi, serikali
haiwezi kukubaliana nayo hivyo amesitisha ujenzi wa jengo hilo.
Majeruhi
waliokumbwa na tukio hilo wameongea na waandishi wa habari japo kwa
taabu na kusema kuwa ukuta uliowaangukia ulikuwa umeunganishwa kama uzio
hivyo wakati wakiendelea kuchimba msingi, uzio huo ulikuwa ukiendelea
kutitia hivyo kusababisha kuporomoka na kuwaangukia.
Daktari
wa zamu wodi ya dharura, Ernest Elisenguo amethibitisha kupokea majeruhi
watano ambao wametokana na tukio la kuporomokewa na kifusi na kuwataja
kuwa ni Ramadhan Hussein Nyarandu, Rashid Mkumba Hamis, Elias Bahati,
Benson Agustino na Mtani ambapo watatu kati ya hao hali yao imeendelea
vizuri na wameruhusiwa kwenda nyumbani ila wawili kati yao bado hali zao
siyo nzuri na wataendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Majeruhi
Rashid Mkumba Hamis, ameeleza kama ifuatavyo: "Mimi ni fundi na
nilikuwa natengeneza 'bezi' kwa ajili ya kushikilia nguzo za ghorofa
wakati ninaendelea na kazi yangu nikaanza kusikia udongo ukiniangukia
mgongoni, ghafla nikasikia matofali yananiangukia.
Katika
kujiokoa matofali yakawa yameniangukia kwenye miguu na bahati mbaya kwa
mujibu wa madaktari ni mwamba nimevunjika mguu ila namshukuru mungu
kuona niko salama."