CCM KUMTEUA MGOMBEA URAIS ANAYEKUBALIKA NA WENGI, KIPENGA KUPULIZWA JUNI
| A |
FILIMBI
kwa ajili ya kuanza kampeni za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais, itapulizwa rasmi
Juni mwaka huu.
Katika
hatua nyingine, chama hicho kimesema kitasikiliza sauti ya wengi katika
kumteua mgombea wa urais, wabunge na madiwani katika Uchaguzi Mkuu
ujao, ilimradi mgombea atakayepaziwa sauti na wengi awe na sifa stahili.
Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema hayo jana alipozungumza na
wajumbe wa halmashauri ya Jimbo la Same Magharibi akiwa ziarani wilayani
humo kushiriki na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katibu
Mkuu huyo wa CCM alisema kutokana na ratiba hiyo, hakuna ruhusa kwa
mwanaCCM yeyote kuanza kampeni kabla ya muda huo, kwa vile hatua hiyo
itatibua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kipindi cha uongozi
kilichosalia.
“Tuwaache
madiwani na wabunge waendelee kufanya kazi zao. Madiwani na wabunge
wengi wanafanya kazi nzuri, ndio maana tunaona miradi mingi
inatekelezwa, tukianza kampeni tutawachanganya na hawatafanya kazi zao
kikamilifu,” alisema Kinana.
Akizungumzia
uteuzi kwa wagombea, Kinana alisema chama hicho kitazingatia maoni ya
wanaCCM wengi katika kumpata mgombea ili kutoa haki kwa vile chama hicho
kimekuwa kikipoteza uongozi katika baadhi ya maeneo kutokana na
kutotenda haki.
“Hili
suala la haki si tu kwamba linasemwa kwa ngazi ya chini, hata sisi
tulio katika ngazi ya juu tunapaswa kuzingatia hili. Sio wanachama wengi
wanasema hivi halafu sisi tunamleta mgombea mwingine, yaani tunapingana
na wapiga kura ambao ni wengi.
“Mgombea
atakayekubalika na wengi ndiye atakayepitishwa ili mradi tu awe na sifa
zinazostahili,” alisema Katibu Mkuu huyo wa CCM.
Alishauri
wanachama na wananchi wa Jimbo la Same Magharibi, kuwachagua tena
madiwani na Mbunge, Dk Mathayo David Mathayo, kutokana na kazi kubwa
waliyoifanya ingawa alisisitiza kuwa hiyo haiondoi haki kwa wanaCCM
wengine kujitokeza kugombea.
“Unajua
kuna haki lakini pia kuna busara katika kuchagua viongozi. Haki ni kwa
mwanaCCM yeyote kujitokeza kugombea, lakini wakati mwingine busara
inatumika kupima kile alichofanya kiongozi aliyepo madarakani katika
kuwaletea maendeleo, na hivyo kustahili kuchaguliwa tena,” alisema
Kinana