WAZIRI WASIRA KUONDOLEWA NYUMBA ANAYOISHI
Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeiagiza Bodi ya Sukari Tanzania
(SBT) kumwondoa katika nyumba ya bodi hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira kutokana na kuishi katika
nyumba hiyo kinyume na taratibu.
Wasira
akiwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika alikuwa akiishi katika
nyumba hiyo inayomilikiwa na SBT iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa SBT, Henry Semwaza aliieleza Kamati ya PAC jana katika
kikao kilichofanyika kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam,
kuwa wamekuwa wakifanya jitihada za kuwasiliana na Wasira kuhusu
kuirejesha nyumba hiyo, lakini hakuna utekelezaji wowote unaofanyika.
“Mara
ya mwisho tulimwandikia barua mwaka 2012 kuhusu kuirejesha nyumba hiyo,
lakini bado hajairejesha na anaendelea kuishi katika nyumba hiyo,”
alisema Semwaza.
Mwenyekiti
wa PAC, Zitto Kabwe akitoa azimio la Kamati hiyo alisema, “Hapa hakuna
msukumo mnaoufanya yaani tangu mwaka 2012 mlipomwandikia barua mpaka
sasa kimya. Tunaiagiza SBT kumwandikia barua Wasira mkimtaka arejeshe
nyumba na nakala ya barua hiyo tuipate Jumatatu (Januari 19 mwaka huu).”
Alisema
kutokana na kuwapo kwa harakati za kutaka kubadili hati ya umiliki ya
nyumba hiyo, Zitto alisema, “Msajili wa Hazina kamati inakuagiza
uhakikishe umiliki wa nyumba hiyo unabaki kwa bodi ya sukari na si
vinginevyo.”
Zitto
pia alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika,
Sophia Kaduma amwandikie barua Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu uamuzi huo wa
Kamati.
Pia,
PAC imeishauri Wizara ya Kilimo kuandaa sheria itakayounda Bodi ya
Sukari isiyokuwa na mgongano wa kimaslahi ili kutoa fursa ya kufanya
uamuzi tofauti na ilivyo sasa.